Waziri wa usalama wa kitaifa nchini Kenya, Profesa Kithure Kindiki, ametoa tahadhari kwa waandamanaji, dhidi ya kufanya maandamano ya vurugu na kuharibu mali.
Tangazo la Kindiki linakuja siku mbili kabla ya maandamano ambayo yameitishwa na upinzani nchini humo siku ya Jumatano Julai 26, kupitia muungano wa Azimio la Umoja- One Kenya.
Waziri huyo wa usalama wa kitaifa amesema katika maandamano ya hapo awali, kulishuhudiwa vifo, vurugu, uporaji na uharibifu wa mali, na hivyo kuondoa dhana ya kuwepo kwa maandamano ya amani.
Profesa Kindiki amesema wizara yake ina jukumu la kuhakikisha nchi iko salama, akiwataka wanasiasa kupingana kupitia sera.
Akizungumza alipozuru jimbo la Baringo kutathmni hali ya usalama katika eneo hilo, Kindiki amewahakikishia wakazi wa Baringo kusini kuwa maafisa wa usalama wataendelea kuwa macho kuhakikisha kuwa majambazi na wahalifu waliojihami hawajipanga tena ili kusababisha ghasia na ugaidi.
Eneo hilo katika Bonde la Ufa, limekuwa likikabiliwa na utovu wa usalama unaosababishwa na wezi wa mifugo.
Wiki iliyopita upinzani ulitangaza maandamano ya siku tatu kuanzia Jumatano hadi Ijumaa, na baada ya kutathmini matukio ya juma lilopita,wamesema hawana nia ya kufanya mazungumzo yoyote na serikali.
Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR imeendelea kutoa kutoa wito wa kuwepo kwa utulivu na kuhimiza mazungumzo ya wazi ili kushughulikia malalamiko ya kijamii, kiuchumi na kisiasa, kwa lengo la kupata suluhu ya kudumu kwa maslahi ya Wakenya wote.”