Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umeanza kutoa mafunzo kwa Madaktari na Wakufunzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi (Vocational Institutes) ili kutoa huduma kwa wanufaika wa Mfuko kwenye Fao jipya la Utengamao.
Hayo yamedokezwa na Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma wakati akifungua mafunzo hayo ya siku tatu yanayofanyika mjini Kibaha ambayo yamewaleta pamoja washiriki kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Akifafanua amesema, Fao la Utengamao limegawanyika katika makundi matatu, Utengamao unaoambatana na matibabu, Utengamao wa Ujuzi (Vocational Rehabilitation) na Utengamao wa Kijamii (Social Rehabilitation).” Amefafanua.
Hata hivyo amesema Fao la Utengamao unaoambatana na matibabu limekwua likitolewa na Mfuko isipokuwa makundi mawili ya Fao la Utengamao wa Ujuzi na Utengamao wa Kijamii.
“Taratibu za Kisera za kutoa fao hili ziko katika hatua za mwisho, Waziri mwenye dhamana ameshapitisha Kanuni na Mfuko tayari una miongozo ya kutoa fao hili na kinachofanyika leo ni kuandaa wataalamu ambao ni ninyi mtakaowahudumia wanufaika wa Mfuko.” Amefafanua.
Akieleza zaidi alisema, endapo mtu amepata ulemavu wa kudumu unaomsababisha ashindwe kufanya kazi aliyokuwa anafanya hapo awali, kupitia fao la utengamao wa ujuzi, anapewa mafunzo hya ujuzi mbadala utakaomsaidia kufanya kazi nyingine, alifafanua Dkt. Mduma.
Aidha kuhusu Fao la Utengamao wa Kijamii, unafafanua jinsi Mfuko unavyoweza kumsaidia Mnufaika kuweka miundombinu rafiki sehemu anakoishi ili kupunguza changamoto zinazosababishwa na ulemavu alionao.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini, WCF, Dkt. Abdulsalaam Omar , amesema washiriki wanatoka katika kada za Udaktari, Wataalamu wa Mazoezi Tiba, Wataalamu wa Viungo Saidizi na Wakufunzi kutoka Vyuo vinavyotoa Huduma ya Utengamao ya Mafunzo ya Ujuzi.
Aidha mshiriki wa mafunzo hayo kutoka Hospitali ya CCBRT ya jijini Dar es S alaam ambae ni Mkuu wa Kitengo cha Utengamao amesema, wanapotekeleza wajibu huo wanapaswa kuwadodosa wateja wao wanaowapatia huduma za utengamao ili kujua taarifa zaidi za changamoto zinazowakabili.