Mshambuliaji mpya wa Inter Milan Lukas Podolski amemshutumu kocha wake Arsene Wenger kwa kitendo cha kutomheshimu baada ya kocha huyo kushindwa kumuaga wakati alipokuwa anakwenda kujiunga na Inter Milan.
Podolski akionyesha dhahiri kutofurahishwa na kitendo hiki amemshushia lawama mzee Wenger akidai kuwa kocha huyu alishindwa hata kumpa neno la kwaheri na kumtakia kila la kheri huko aendako kama ilivyo kwa mtu mstaarabu.
Kauli hii inathibitisha uhusiano mbovu ambao umekuwepo kati ya Wenger na Podolski baada ya mshambuliaji huyu kunukuliwa hapo awali akisema kuwa Wenger hampi nafasi ya kutosha kuonyesha uwezo wake.
Lukas Podolski hakuwahi kupewa nafasi kwenye kikosi cha kwanza kwa muda wote aliokuwa Arsenal hali iliyochangia nyota huyo kupelekwa Italia kuichezea Inter Milan kwa mkopo.
Kufuatia kauli hii inaonekana wazi kuwa kuna uwezekano mkubwa wa Podolski kutorejea Arsenal hata baada ya kumalizika kwa mkataba wake wa mkopo wa miezi 6 ambao anautumikia Inter Milan.