Katika kambi ya wakimbizi iliyoko katika mji wa Adre nchini Chad, makumi ya akina mama wanasubiri na watoto wao wagonjwa nje ya hospitali moja ya kambi hiyo.
Wafanyakazi wa misaada katika kambi hiyo walilalamikia ukosefu wa dawa na wakaomba msaada wa haraka wa matibabu. “Mgonjwa yeyote mwenye utapiamlo anayekuja kwetu anapaswa kupokea dawa zinazofaa na hatuna dawa yoyote hapa,” alisema daktari wa kujitolea, Hashem Moussa.
Takriban watoto 500 wamekufa kutokana na njaa nchini Sudan – ikiwa ni pamoja na watoto dazeni wawili katika kituo cha watoto yatima kinachosimamiwa na serikali katika mji mkuu wa Khartoum – tangu mapigano yalipozuka, Save the Children lilisema Jumanne.
Kulingana na kundi la misaada, kwa uchache watoto 31,000 wanakosa matibabu ya utapiamlo na magonjwa yanayohusiana nayo tangu shirika hilo la misaada lililazimishwa kufunga vituo vyake 57 vya lishe nchini Sudan.
Sudan ilitumbukia katika machafuko mwezi Aprili wakati mvutano mkali kati ya wanajeshi, wakiongozwa na Abdel Fattah Burhan, na RSF, wakiongozwa na Mohammed Hamdan Dagalo, ulilipuka na kusababisha mapigano ya wazi katika mji mkuu, Khartoum, na kwingineko.
Zaidi ya watu milioni 3.4 walilazimika kuyahama makazi yao hadi maeneo salama ndani ya Sudan, kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji. Zaidi ya milioni moja walivuka kwenda nchi jirani, ikiwa ni pamoja na Misri, Chad, Sudan Kusini, Ethiopia na Jamhuri ya Afrika ya Kati, kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji.
Shirika hilo lilisema kuwa zaidi ya wakimbizi 414,000 wamekimbilia Chad tangu mzozo huo uanze mwezi Aprili, huku wimbi kubwa la watu likionekana hivi karibuni huku mapigano yakizidi kuongezeka huko Darfur.
Mzozo huo umegeuza Khartoum na maeneo mengine ya mijini kuwa uwanja wa vita. Wakazi wengi wanaishi bila maji na umeme, na mfumo wa huduma za afya nchini umekaribia kuporomoka.
Eneo linalosambaa la Darfur lilishuhudia baadhi ya matukio mabaya zaidi ya ghasia katika mzozo huo, na mapigano huko yamebadilika na kuwa mapigano ya kikabila na RSF na wanamgambo washirika wa Kiarabu wanaolenga jumuiya za kikabila za Kiafrika.