Baadhi ya Wazee wenye ugonjwa wa Ngirimaji unaosababisha korodani kujaa maji (Mabusha) Wilayani Pangani Mkoani Tanga wamemuomba Mkuu wa Wilaya hiyo Zainab Abdallah @zainababdallah93 kuangalia uwezekano wa kubadilishwa kwa Watoa huduma wa afya wanaowatibu ili wawe Wanaume na sio Wanawake huku wakisema wapo tayari Mabusha yawaue tu lakini hawataki kutomaswa na Wasichana.
Akiongea kwa niaba ya Wazee hao katika ziara ya ‘Twende na Samia Kijiji kwa Kijiji’ ya DC Zainab, Mzee Ebiati Mpambajoto amesema Serikali huwa inatoa fursa za matibabu kwa Wazee wenye Mabusha lakini wengi wao wamekuwa wakitoroka Hospitali wakati wakiandaliwa kufanyiwa upasuaji kutokana na kuandaliwa na watoa huduma wa kike ambao wengine ni wadogo jambo ambalo Wazee hao wanaona linawashushia heshima na kuwafedhehesha.
“Serikali imekuwa na utaratibu mzuri wa kutoa matibabu kwa sisi wenye Mabusha lakini unakuta Mzee anaenda na mzigo wake kule inafika mahali anamkuta Binti ndio anamtomasa, ebu niambie huyo Mtu akitoroka Hospitali unamlaumu nani?, Mimi nitakubali nikafe na mzigo wangu kuliko Binti mdogo anikamatekamate mimi naondoka kweli na nikija kufa huku Serikali ya Rais Samia itapata lawama”
“Inakuwaje Mzee wa kiume akubali kushikwashikwa na Mtoto mdogo wa kike inaingia akilini? au sasa hivi haki ipo kwa Wanawake sisi hatuna haki?, mbona Wanawake hawakamatwi na Askari wa kiume?”
Kwa upande wake DC Zainab amemuomba Mganga Mkuu wa Wilaya kufanyia kazi malalamiko ya Wazee hao kwa kuzingatia maadili na miiko ya utoaji huduma za afya.