Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja amezitaka taasisi zilizochini ya wizara hiyo kutumia Makumbusho za Taifa kama eneo mojawapo la kuiongezea Serikali mapato.
Masanja ametoa maelekezo hayo Machi 6, 2023 katika Ukumbi wa Ofisi za Ngorongoro zilizopo Jijini Arusha wakati akiongoza kikao cha kimkakati cha kufanya mapitio ya taarifa mbalimbali za utendaji kazi za Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa lengo la kuboresha utendaji kazi na hatimaye kukuza utalii na kuimarisha usimamizi wa Uhifadhi wa Maliasili nchini.
Masanja ametumia fursa hiyo kuwataka watendaji wa Taasisi kuwa wabunifu kwa kutumia historia ya taifa na elimu ya viumbe hai kuwa fursa ya kujifunza na kuiongezea Serikali Mapato na kuongeza ajira na kipato kwa Mwananchi mmoja mmoja.
Katika hatua nyingine,Masanja amekielekeza Chuo cha FITI kuandaa mpango utakaokiwezesha Chuo hicho kuwepo na miradi mbalimbali itakayokiwezesha kuongeza mapato kwa njia ya Mafunzo.
Taasisi zilizoshiriki kikao hicho ni Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), Chuo cha Viwanda vya Misitu (FITI), Makumbusho ya Taifa ( NMT) pamoja na watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.