Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya kwamba bila hatua za haraka, zaidi ya watoto milioni moja watapata utapiamlo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Akielezea hali ya sasa nchini DRC kama “janga,” afisa mkuu wa dharura wa WHO Adelheid Marschang aliambia mkutano wa Umoja wa Mataifa huko Geneva siku ya Ijumaa kwamba hali ni mbaya zaidi katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.
“Katika miezi iliyopita, DRC imekabiliwa na kuongezeka kwa migogoro na ghasia, na kusababisha watu wengi kuhama makazi yao, magonjwa kuenea, unyanyasaji wa kijinsia, na kiwewe kikubwa cha akili, haswa katika eneo la mashariki mwa nchi,” Marchang alisema.
Alibainisha kuwa nchi hiyo ina “idadi kubwa zaidi ya watu wanaohitaji misaada ya kibinadamu” duniani kote, na watu milioni 25.4 wameathirika.