Mkurugenzi Mtendaji wa Operesheni za Dharura wa Ofisi ya Kikanda ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ameelezea hali ya Libya kuwa janga baada ya dhoruba na kimbunga kikali kilichoikumba nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Richard Brennan ameonya kuwa: “Hali ya Libya baada ya kimbunga kilichosababisha uharibifu mkubwa kwa ujumla hasa katika mji wa “Derna”, ni janga kubwa.
Mkurugenzi Mtendani wa Operesheni za Dharura wa Ofisi ya Kikanda ya Shirika la Afya Duniani, ameeleza kuwa hakukutarajiwa maafa makubwa kama hayo nchini Libya, na kuongeza kuwa: “Operesheni za uokoaji zinaendelea ingawa uwezekano wa kupata manusura unafifia.”
Brennan ameendelea kusema kuwa: “WHO ina wasiwasi juu ya uwezekano wa kusambaa magonjwa ya mlipuko, haswa kwa watoto, na tatizo kubwa nchini Libya ni kupata timu maalumu za wataalamu kwa ajili ya kutumwa katika maeneo yaliyoathiriwa.”
Mafuriko makubwa yaliyoikumba Libya tarehe 10 September yamesababisha maafa ikiwemo vifo vya takriban watu 3,000 na wengine zaidi ya 10,000 hawajulikana waliko Mashariki mwa nchi hiyo.
Kimbunga hicho pia kilisababisha kukatika kwa mawasiliano, kuanguka kwa nguzo za umeme na miti na mafuriko kusambaa pia katika miji mingine.
Maeneo yote ya mji wa Derna Mashariki mwa nchi hiyo yamemezwa na maji sambamba na wakazi wa maeneo hayo na kufanya hali kuwa ya taharuki, janga kubwa lisilohimiliwa.
Serikali ya Libya imetangaza siku tatu za maombolezo katika maeneo yote yaliyoathirika.