Zaidi ya raia 370 wa Zambia wamefariki dunia na wengine 9,580 wamepata maambukizi ya maradhi ya kipindupindu yanayotajwa kuwa na uwezo wa kusababisha vifo ndani ya saa chache.
Ndani ya siku chache ziizopita, nchi hiyo ilitangaza kuwa ilirekodi visa vipya 418 na vifo 12 idadi ambayo waziri wa afya Sylvia Masebo ameielezea kuwa ni ya kushtusha.
Badala ya shule na vyuo kufunguliwa Januari 8 kama ilivyokuwa hapo awali, na sasa taasisi hizo za elimu zitafunguliwa Januari 29 wakati serikali ikiendeleza juhudi zake za kupambana na ugonjwa huo. Mikoa tisa kati ya 10 ya nchi hiyo imeathiriwa na kipindupindu.
Taifa hilo limetangaza kuwa limepokea dozi milioni 1.4 za chanjo dhidi ya ugonjwa wa kipindupindu kutoka shirika la Afya Duniani WHO, ili kukabiliana na maradhi hayo ya mlipuko yaliyoanza kuitikisa nchi hiyo ya kusini mwa bara la Afrika tangu mwezi Oktoba mwaka uliopita.
Wakati alipokuwa akikabidhi chanjo mjini Lusaka, Mratibu Mkaazi wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Cissy Byenkya amesema kuwa shirika hilo linashirikiana vilivyo na serikali ya Zambia kukabiliana na tatizo hilo.