Kwaajili ya maendeleo ya familia na jamii kwa ujumla, wazazi na walezi wametakiwa kuunga mkono elimu kwa watoto wa kike ili kuwajengea ujasiri na kuchukua nafasi za uongozi wa juu.
Wito huo umetolewa na Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) ambayo ni kampuni tanzu ya AngloGold Ashanti, iliyowakilishwa na Elizabeth Karua, Mwanasheria wa GGML, kwenye jopo la Mkutano wa Uongozi wa Wanawake katika Usimamizi Afrika (WIMA) ulioandaliwa kwenda sanjari na Siku ya Wanawake Duniani.
Mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam katika wmkesha wa Siku ya Wanawake Duniani 2024 chini ya ufadhili wa GGML, ulijumuisha mada mbalimbali ikiwemo ushiriki wa wanawake katika changamoto za uongozi, biashara na mazingira.
Katika mchango wake kwenye mjadala huo, Mwanasheria wa GGML, Elizabeth Karua, alisema ili kuongeza ushiriki wa wanawake katika sekta ya uchimbaji madini, kampuni inatoa kipaumbele kwa wanawake kutuma maombi ya ajira na mchakato wa kuajiri unazingatia uwiano wa jinsia wa 50/50 kwenye kundi la waliotuma maombi ya ajira.
“Mazingira ya kazi katika GGML yanabaki kuwa ya kirafiki kwa wanawake, hasa ukizingatia wanapata vyeo vya juu ndani ya GGML huku wengine wakivuka mipaka na kuwa wakuu wa idara hiyo katika makampuni mbalimbali nje ya nchi,” alisema.
Kwa upande mwingine, Meneja wa Mahusiano ya Umma na Mawasiliano wa GGML, Stephen Mhando, alisema mgodi huo unaoongoza kitaifa katika kutoa fursa kwa wanawake katika sekta ya uchimbaji nchini.
Alisema asilimia 13 ya wafanyakazi wa mgodi huo ni wanawake wengi wao wakiwa wanafanya kazi kwenye nafasi za usimamizi, hali inayochochea wanawake wengine kujiunga na sekta ya uchimbaji.
“GGML, ambayo imeendelea kudhamini miradi ya kuwawezesha wanawake ikiwa ni pamoja na WIMA, inajivunia kuonyesha jinsi tunavyojali wanawake na kufanya kazi nao kwa karibu. Ikiwa utalinganisha tulikotoka na tulipo sasa, ni hatua kubwa kwa sababu ingawa tunaweza kuwa na wanawake wachache, wako kwenye nafasi ambazo wanawaongoza watu,” alisema.
Mgeni rasmi wakati wa mkutano huo, Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, Profesa Marcellina Mvula Chijoriga, aliwasihi wazazi kuwekeza katika elimu ya mtoto wa kike kwani elimu ndiyo itakayomwezesha kushiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi.
“Wito wangu kwa akina mama na akina baba, elimisheni binti yenu vizuri… ili aweze kwenda mbali, ukiwekeza kwa binti, umewekeza kwenye familia na jamii kwa ujumla,” alisema.
Pia aliwasihi wanawake kujifunza kufanya kazi pamoja na kuchukua nafasi za uongozi.
“Ujasiri wangu ndio ulioniruhusu kufanya kazi na marais wanne. Nguvu yako inatoka kwako. Namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuniteua kuwa mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere,” alisema.
Kwa mujibu wa Naike Moshi, Afisa Mtendaji Mkuu wa WIMA, changamoto kubwa kwa wanawake bado ni ukosefu wa fursa ya elimu.
Alisema kwakuwa asilimia 32 pekee ya wasichana ndio wanaomaliza shule ya sekondari, bado kunahitajika msukumo mkubwa unahitajika kwa wazazi na walezi kumsomesha mtoto wa kike.
Women In Management Africa (WIMA) ni mpango unaolenga kuwaendeleza wanawake kupitia mafunzo ya uongozi na ushauri, kutoa nafasi salama kwa mtandao na kubadilishana mawazo na wasiwasi. Mpango huo pia unakuza kikamilifu usawa wa kijinsia na kuhimiza ushiriki wa wanawake katika nguvu kazi kwa kuwaheshimu wanawake wenye taaluma katika taaluma zao na kuwahamasisha wanawake zaidi kuchukua nafasi za uongozi mahali pa kazi.