Wizara ya afya katika Ukanda wa Gaza unaotawaliwa na Hamas siku ya Jumatatu ilisema takriban watu 28,340 wameuawa katika eneo hilo lililozingirwa wakati wa vita kati ya wanamgambo wa Kipalestina na Israel.
Idadi ya hivi punde ni pamoja na vifo 164 katika muda wa saa 24 zilizopita, taarifa ya wizara ilisema, wakati jumla ya watu 67,984 wamejeruhiwa huko Gaza tangu kuanza kwa vita mnamo Oktoba 7.
Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni Tedros Adhanom Ghebreyesus Jumatatu alisisitiza wito wa kusitishwa kwa mapigano huko Gaza na kuelezea wasiwasi wake hasa juu ya mashambulio ya Israeli huko Rafah ambapo wakaazi wengi wa eneo hilo wamekimbia.
Mashambulizi ya anga ya Israeli usiku kucha yaliwauwa watu 48 huko Rafah, mamlaka ya afya ya eneo hilo ilisema.
Ghebreyesus alisema ni hospitali 15 tu kati ya 36 huko Gaza “zinazofanya kazi kwa sehemu au kidogo” na kwamba wafanyikazi wa misaada wanafanya bidii yao katika hali ngumu.