Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kuimarisha ubora wa huduma za Afya ya mama na mtoto katika vituo 25 vinavyotoa huduma ya upasuaji wa dharura wa kumtoa mtoto tumboni (CEmONC) katika Mkoa wa Dar Es Salaam ili kupunguza vifo vitokanavyo na Uzazi.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo leo Machi 28, 2024 wakati akifungua mafunzo elekezi kazini juu ya huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto katika Mkoa wa Dar Es Salaam ambapo mafunzo hayo ni endelevu yanayotolewa nchini nzima ili kupunguza vifo vya mama mjamzito na mtoto.
“kuimarisha ubora wa huduma za Afya ya mama na mtoto katika vituo 25 vya Afya vinavyotoa huduma ya upasuaji wa dharura wa kumtoa mtoto tumboni yaani (CEmONC) tutakua tumetatua asialimia 84 ya changamoto za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto kwa Mkoa wa Dar Es Salaam.” Amesema Waziri Ummy.
Amesema, mafunzo haya ni muhimu sana ambayo yamesaidia kupunguza vifo katika katika Mkoa wa Tabora ambapo kwa mwaka 2023 vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka vifo 50 hadi vifo Vinne kwa miezi Mitatu, lakini pia mafunzo hayo yanasaidia kupeana mbinu mbalimbali za kuwahudumia vizuri wagonjwa ili kuendelea kupunguza vifo vitokanavyo na Uzazi.
“Mkoa wa Dar Es Salaam kwa Mwaka 2023 kulikua na vifo vya wajawazito 219, vifo vya watoto wachanga 1,701 hivyo tunaamini kupitia mafunzo haya tutapunguza takwimu hizi za vifo kwa zaidi ya asilimia 50, inawezekana.” Amesema Waziri Ummy
Aidha, Waziri Ummy amezitaka Halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya kuwawezesha watoa huduma waliopatiwa mafunzo hayo ili waweze kwenda kutoa mafunzo hayo kwenye vituo vyao vya Afya vinavyotoa huduma ya upasuaji wa dharura wa kumtoa mtoto tumboni (CEmONC) vilivyobakia pamoja na Zahanati.
Pia, Waziri Ummy amezitaka kila Hospitali pamoja na Vituo vya Afya vinavyotoa huduma ya upasuaji wa dharura wa kumtoa mtoto tumboni (CEmONC) zianzishe wodi maalumu ya watoto wachanga inayofanya kazi kwa kuwa na vifaa tiba pamoja na watoa huduma waliojengewa uwezo.