Wizara ya Katiba na sheria imetoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Njombe wenye uhitaji wa huduma ya msaada wa kisheria kujitokeza katika maeneo yao yatakayopangwa kwa ajili ya kupata huduma hiyo bure.
Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Dkt. Pindi Chana ametoa wito huo leo Mei 22, 2024 wakati akizungumza na Waandishi wa habari katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe juu ya uzinduzi wa kampeni ya Msaada wa Kisheria maarufu kama “Mama Samia Legal Aid Campaign” itakayo fanyika mkoani humo kuanzia Mei 26,2024 katika viwanja vya kituo cha zamani cha mabasi cha Njombe mjini.
“Na mgeni rasmi wa shughuli hii ya uzinduzi rasmi atakuwa ni Mhe Dotto Biteko Naibu Waziri mkuu na Waziri wa Nishati,nitumie nafasi hii kuwaalika wananjombe wakaribie kwa ajili ya kupata msaada wa kisheria,tunafahamu wananchi wanachangamoto hivyo milango iko wazi”amesema Pindi Chana.
Vile vile ameongeza kuwa “Kampeni hii itatekelezwa katika halmashauri zote za mkoa wa Njombe ikijumuisha kata stini na vijiji mia na themanini kwa kipindi cha siku kumi na huduma hizo zitatolewa na timu za wataalamu wa taasisi za serikari na zisizo za serikali”
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Njombe Anthony Mtaka amesema wamejiandaa kikamilifu katika kuhakikisha kuwa wananchi wa Tanzania wananufaika na Kampeni hiyo.
“Wananchi wote wenye malalamiko ambayo wanaona yanahitaji msaada wa kisheria tutumie wiki hii vizuri kwa kufika kwenye maeneo ambayo huduma hii inatolewa”amesema Mtaka
Utekelezaji wa Kampeni hiyo ulianzia jijini Dodoma ambapo ilizinduliwa tarehe 27 Aprili, 2023, na Zanzibar tarehe 9 Mei, 2023 ambapo Kwa sasa Kampeni hii imeufikia mkoa wa Njombe.