Wizara ya Maliasili na Utalii imevunja rekodi kwa kukamilisha ujenzi Jengo jipya la Ofisi lililopo kwenye Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma, na kuruhusu sasa Jengo hilo kutumika rasmi.
Akipokea Jengo hilo, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi amesema kukamilika vyema na kwa wakati kwa Jengo hilo, ni matokeo chanya ya juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha huduma kwa wananchi pamoja na sekta nzima ya Maliasili na Utalii ili sekta hiyo iwanufaishe vyema watanzania.
Dkt. Abbasi amewapongeza wote walioshiriki kikamilifu katika ujenzi wa Jengo hilo pamoja na menejimenti ya Wizara hiyo kwa usimamizi wa karibu wa kila hatua katika kuhakikisha linakamilika kwa wakati na kwa ubora uliokusudiwa huku akitoa rai kwa watumishi watakaotumia Jengo hilo kuhakikisha linatunzwa kikamilifu.
Awali akitoa Taarifa juu ya ujenzi wa Jengo hilo, Mshauri elekezi kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), Mhandisi Lupakisyo Mealwiba amesema Jengo hilo, lililogharimu Bilioni 17,299,544,788.02 za kitanzania lina urefu wa mita 88, upana mita 14.9, pamoja na mambo mengine jengo hilo lina vyumba 118 vya Ofisi ikihusisha Ofisi za viongozi wakuu wa Wizara.
Jengo hilo lenye kuvutia na kuweka Historia isiyofutika kuwa jengo la kwanza kukamilika kujengwa kati ya Majengo ya Wizara mbalimbali za Serikali, limejengwa na Mkandarasi anaeitwa M/S. LI JUAN Development Construction CO.LTD ya nchini China.