Viongozi wa Wizara ya Nishati pamoja na ujumbe wa Wataalam kutoka Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) wamefanya kikao kazi kuhusu utekelezaji wa mradi wa kujengea uwezo Wizara ya Nishati, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) katika masuala ya kusanifu mitandao ya usambazaji wa Gesi Asilia.
Kikao hicho kilifanyika tarehe 26 Oktoba 2023 jijini Dodoma ambapo mradi huo wa kusanifu mitandao ya Gesi Asilia unahusisha Mkoa wa Dodoma, Pwani na Dar es Salaam.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Petro Lyatuu alisema kuwa, mradi huo kwa upande wa Tanzania una umuhimu mkubwa kwani utasaidia matumizi ya uhakika ya Gesi Asilia.
Lyatuu alizitaja faida za mradi huo ambazo ni pamoja na kuongeza utalaam kwa wazawa kutokana na mafunzo mbalimbali yatakayotolewa katika masuala ya kuendesha miradi ya Gesi Asilia nchini ambapo nchi itaongeza pia idadi ya watalaam kutokana na mafunzo hayo.
Aliongeza kuwa, katika kipindi hiki ambacho nchi ipo kwenye mkakati wa kuingia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia, mradi huo wa kuwajengea uwezo wataalam katika masuala ya Gesi Asilia utasaidia pia katika kutekeleza mkakati huo.
Alisema, Rais Samia aliagiza kuandaa mkakati wenye lengo la kuhakikisha asilimia 80 kuweza kutumia nishafi safi ya kupikia ifikapo mwaka 2033 na hivyo mradi huu utawezesha lengo hilo kufanikiwa kwa haraka.
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkuu wa JICA Ofisi ya Tanzania, Hitoshi Ara, aliishukuru Wizara kwa ushirikiano waliotoa kutoka mwanzo wa makubaliano ya utekelezaji wa mradi huo na kuahidi kuwa Shirika hilo litaendelea kutoa ushirikiano kwa Wizara pale itakapohitajika.