Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuanzia mwaka wa fedha ujao 2024/25 kupitia Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) wizara hiyo inatarajia kuanzisha mtaa wa viwanda kwa kila wilaya ili wafanyabiashara wadogo waweze kuchakata mazao yanayopatikana katika maeneo yao.
Dkt. Kijaji amesema hayo wakati akihitimisha hoja ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25 ambapo amesema mtaa huo ni sehemu programu ya BBT- Viwanda(Building a Better Tomorrow) kama inayotekelezwa na wizara ya Kilimo kwaajili ya kuwawezesha wafanyabiashara wadogo.
“USAID mkataba wa biashara tuliosaini nao wanatusapoti kwenye eneo hili na tutapita kwenye maeneo ya wabunge(majimboni) ili tukubaliane tunaweka wapi mtaa huo wa viwanda ili kila wilaya iweze kuchakata malighafi zinazopatikana kwa wingi kwenye wilaya hiyo” Dkt. Ashatu Kijaji – Waziri wa Viwanda na Biashara