Leo April 23, 2018 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema msanii Wema Sepetu na wafanyakazi wake wanaokabiliwa na tuhuma za kutumia dawa za kulevya wana kesi ya kujibu, hivyo wataanza kujitetea.
Uamuzi huo, umetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya wakili wa serikali, Constantine Kakula kueleza kuwa kesi hiyo imeitishwa kwa ajili ya uamuzi kama washtakiwa wana kesi ya kujibu ama lah.
Katika uamuzi wake Hakimu Simba amesema kwa mujibu wa sheria kama washtakiwa wakipatikana na kesi ya kujibu watatakiwa kujitetea, pia kama hawana kesi ya kujibu wataachiwa huru.
“Baada ya kupitia hoja zote, mahakama imejitosheleza kwamba washtakiwa wote wana kesi ya kujibu katika mashtaka yote, hivyo wana haki kisheria kuanza kujitetea,” amesema Hakimu Simba.
Baada ya kusema hayo, Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi May 14 na 15,2018 ambapo washtakiwa watajitetea mfululizo.
March 23,2018 upande wa utetezi kupitia wakili Alberto Msando, uliwasilisha hoja katika mahakama hiyo kwamba washtakiwa hawana kesi ya kujibu.
Mbali na Wema washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ya kutumia dawa za kulevya ni Angelina Msigwa na Matrida Seleman Abbas.
Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kukutwa na kiwango kidogo cha dawa za kulevya na kutumia dawa za kulevya.
Inadaiwa kuwa February 4,2017 katika Makazi ya Wema huko Kunduchi Ununio washtakiwa hao walikutwa na msokoto mmoja na vipisi vya bangi vyenye uzito wa gramu 1.08.
Kwa upande wa Wema yeye anadaiwa kuwa February Mosi, 2017 katika eneo lisilojulikana jijini Dar es Salaam, alitumia dawa za kulevya aina ya Bangi.