Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu inatarajia kutoa uamuzi April 23,2018 kuhusu kesi ya kutumia dawa za kulevya inayomkabili mrembo Wema Sepetu na wenzake kama wana kesi ya kujibu ama hapana.
Uamuzi huo unatarajiwa kutolewa na Hakimu Mkazi Mkuu,Thomas Simba baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi watano wa upande wa mashtaka.
March 23,2018 upande wa utetezi kupitia wakili Alberto Msando, uliwasilisha hoja katika mahakama hiyo kwamba washtakiwa hawana kesi ya kujibu.
Mbali na Wema washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ya kutumia dawa za kulevya ni Angelina Msigwa na Matrida Seleman Abbas.
Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kukutwa na kiwango kidogo cha dawa za kulevya na kutumia dawa za kulevya.
Inadaiwa kuwa February 4,2017 katika Makazi ya Wema huko Kunduchi Ununio washtakiwa hao walikutwa na msokoto mmoja na vipisi vya bangi vyenye uzito wa gramu 1.08.
Kwa upande wa Wema yeye anadaiwa kuwa February 1, 2017 katika eneo lisilojulikana jijini Dar es Salaam, alitumia dawa za kulevya aina ya Bangi.