Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imekwama kusikiliza kesi ya mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kwa sababu shahidi wa upande wa mashitaka yupo katika majukumu mengine.
Hatua hiyo inatokana na maelezo ya Wakili wa Serikali, Tumaini Kweka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati shauri hilo lilipoitishwa kwa ajili ya kusikilizwa.
Wakili Kweka amedai kuwa shauri lilipangwa kwa ajili ya kusikilizwa lakini shahidi waliotaka kuendelea naye yupo katika ‘Operation’ hivyo wanaomba ahirisho fupi ili waweze kuendelea na usikilizwaji.
Baada ya kueleza hayo, Wakili wa Zitto, Peter Kibatala hakuwa na pingamizi ambapo shauri imeahirishwa hadi Aprili 24 na 25, 2019.
Katika kesi hiyo, inadaiwa Oktoba 28, 2019 Zitto akiwa katika mkutano na waandishi wa habari, uliyofanyika katika Makao Mkuu ya ofisi ya Chama cha ACT-Wazalendo alitoa maneno ya uchochezi yenye kuleta hisia ya hofu na chuki.