Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mohammed Mchengerwa amesema serikali inatarajia kutoa ajira 23,000 za Walimu na Maafisa Afya hivi karibuni ambapo tayari wizara imeshapata kibari cha kutoa ajira hizo.
Waziri Mchengerwa amebainisha hayo akiwa mkoani Morogoro wakati akifunga Kikao Kazi cha Makatibu Tawala Wasaidizi Elimu na Maafisa wa Elimu wa Halmashauri zote nchini, ambao wamektana kwa lengo la kujadili utekelezaji na uboreshaji wa sekta ya elimu.
Amesema serikali imeendelea kutoa ajira za Ualimu ambapo kwa mwaka 2022/23 jumla ya walimu 13,130 waliajiriwa na kupangiwa kazi katika maeneo mbalimbali hapa nchini, huku akifanikiwa kuwapandisha madaraja walimu 227,263 pamoja na kuwalipa walimu wa ajira mpya stahiki zao.
“Natambua kwamba kwa Mwezi huu wa Jnuary Ofisi ya Rais TAMISEMI tunacho kibali cha ajira na tutangaza hivi punde ajira za Walimu na Maafisa Afya takribani 23,000 wataajiriwa hivi karibuni” Amesema Waziri Mchengerwa
Awali akitaja mafanikio ya Serikali katika uboreshaji wa sekta ya Elimu, Waziri Mchengerwa amesema, serikali imetenga fedha Shilingi Trioni 1.2 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu elimu Sekondari kwa kipindi cha miaka miatno 2021/25 huku serikali ikutumia shilingi Bilioni 33.3 kila mwezi kwa ajili ya elimu bila malipo.