Watathmini wa Serikali wa Madini ya Almas wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kosa la kuisababishia Serikali hasara ya Tsh. Bilioni 2.4.
Vigogo hao ni Mkurugenzi wa Tathmini wa Madini ya Almas, Archard Kalugendo mwenye umri wa miaka 49 na Mtathmini wa Madini, Edward Rweyemamu mwenye umri wa miaka 50.
Kwa pamoja wamesomewa makosa yao na Wakili wa Serikali, Paul Kadushi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage.
Kadushi amedai washtakiwa wanakabiliwa na kosa moja la kuisababishia Serikali hasara, ambapo kosa hilo wamelitenda kati ya August 25 na 31, 2017 katika maeneo ya Dar es Salaam na Shinyanga wakidaiwa kuisababishia Serikali hasara ya Dola za Kimarekani, Milioni 1,118,291.43 ambazo ni sawa na Tsh. Bilioni 2.4.
Baada ya kuelezwa Kadushi amedai upelelezi upo mbioni kukamilika, ambapo Hakimu Mwijage amesema Mahakama hiyo haina mamlaka na maombi ya dhamana wapeleke Mahakama Kuu, hivyo washtakiwa hawaruhusiwi kujibu.
Wakili wa utetezi, Nehemia Nkoko amedai amekaa na wateja wake kwa muda mrefu tangu walipokamatwa na anaamini upelelezi umefanyika mkubwa na sehemu iliyobaki ni ndogo sana, haiwezi kuchukua muda mrefu na wanaomba upelelezi ukamilike haraka.
Baada ya hapo kadushi amedai watahakikisha upelelezi unakamilika kwa wakati.
Hakimu Mwijage amesema upelelezi ukamilike ili mwenye hatia afungwe na asiyekuwa na hatia aachiwe, ambapo ameahirisha kesi hadi September 29, 2017.
Madini ya Bilioni 32 yazuiwa kusafirishwa Airport DSM