Mfanyabiashara Harbinder Sigh Sethi leo September 20, 2017 amewasilisha maombi ya dhamana katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ‘Mahakama ya Mafisadi’.
Sethi amewasilisha maombi hayo namba 29, 2017 katika Mahakama hiyo na kusikilizwa mbele ya Jaji Winfrida Koroso ambapo anatarajia kutoa uamuzi September 26, 2017.
Katika hati ya maombi, Sethi ambaye anawakilishwa na Wakili Joseph Makandege anaomba apatiwe dhamana katika kesi ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha iliyopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Wakili Makandege amedai kuwa June 16, 2017 alikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere akielekea Afrika Kusini kwa matibabu akidai siku hiyo alivyokamatwa alifunikwa uso na kushambuliwa na kupelekwa sehemu isiyojulikana na watu wenye silaha.
Inadaiwa kuwa June 19, 2017 alipelekwa Kituo Kikuu cha Polisi na baadaye alipelekwa Mahakamani siku hiyo hiyo na mtu mwingine ambaye ni James Rugemarila wakikabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi, kula njama, kugushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kujipatia fedha kwa njia ya udanganjifu, kutakatisha fedha na kusababisha hasara.
Makandege alidai July 3, 2017 kabla ya kuomba dhamana upande wa mashtaka ulifanya mabadiliko kwenye hati ya mashtaka na kuongeza mashtaka sita ya utakatishaji fedha.
Kutokana na ushauri wa Wakili Makandege anaamini kuwa makosa ya utakatishaji fedha hayana dhamana lakini katika mazingira kadhaa Mahakama inaweza kuchepuka katika msimamo huo na kutoa dhamana akidai baadhi ya mazingira hayo ni pamoja na Sethi kuwa mgonjwa na kuhitaji uangalizi wa wataalamu bila hivyo kuna uwezekano wa kupoteza maisha na kushindwa kuendelea na mashtaka yanayomkabili.
Pia katika hati ya kiapo alidai alifanyiwa upasuaji Afrika Kusini mara mbili na mwaka huu mara moja ambapo aliwekewa puto tumboni mwake hivyo anahitaji kuwa na mtaalamu wa kumuangalia mara kwa mara.
Alidai 1994/95 alipata ajali ambapo mapafu yake yaliathirika vibaya na ilichukua saa kadhaa kwa madaktari kunusuru maisha yake lakini pia hali hiyo ilijirudia 2015 ambapo mapafu yalishindwa kufanya kazi na kupelekwa Nairobi.
Aidha, kutokana na ugonjwa huo inalazimika kila mwezi kupata matibabu kutoka kwa madaktari wataalamu huko Afrika Kusini ili kuangalia mwenendo wa afya yake na Puto lililoko tumboni mwake.
>>>”Kuna vifaa maalumu vya kitaalamu ambavyo anapaswa kutumia ambavyo vinamsaidia kupumua usiku lakini kwa sasa hawezi kuvipata kwa sababu yuko gerezani.”
Alidai Idara ya Magereza inazuia mahabusu na wafungwa kuwa na vifaa hivyo akiwa gerezani na haina uwezo wa kumpatia vifaa hivyo huku akiomba pia kupatiwa dhamana kwa sababu anao wadhamini wa kuaminika na yuko tayari kutimiza masharti atakayopewa na hajawahi kushtakiwa kwa kosa lolote la jinai.
Alidai mashtaka yanayomkabili hayana vionjo muhimu vya kumfanya abaki mahabusu, lakini hata hivyo Wakili wa Serikali Zainabu Mango ameweka pingamizi kuwa hati ya kiapo iliyowasilishwa ina mapungufu ambapo Jaji Koroso aliahirisha kesi hiyo hadi September 26, 2017 kwa ajili ya kutoa uamuzi.
“Inawezekana Mungu alikosea kuweka Tanzanite kwa Watanzania” – President JPM