Mkazi wa Chato Mkoa wa Geita, Obadia Kiko mwenye umri wa miaka 41, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akituhumiwa kwa kosa la kuchapisha taarifa isiyo sahihi kupitia mtandao wa Facebook.
Mkazi huyo wa jamii ya Kimasai, amesomewa kosa lake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri na Wakili wa Serikali, Leornad Challo ambapo Wakili Challo amedai mshtakiwa anakabiliwa na kosa moja la kuchapisha taarifa ya uongo kupitia mfumo wa kompyuta na kuweka kwenye mtandao wa Facebook, kinyume na sheria ya makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015.
Inadaiwa August 3, 2017 akiwa maeneo ya Chato mkoani Geita, mtuhumiwa alichapisha taarifa iliyosema kuwa: “Taarifa kutoka kikao cha mazungumzo kati ya Serikali na wawakilishi wa Kampuni ya Acacia kuwa wanasheria wetu wanashindwa kutafasiri vifungu vya sheria hadi kufikia kuomba msaada kwa wanasheria wa Acacia, sasa hivi ni vituko mwizi anakusaida sheria hahahaaaa….
#Mazungumzo bado yanaendelea lakini wanasheria wetu wanabanwa sana ukizingatia wale jamaa wanavielelezo vyote vya mikataba kiukweli tumuombe Mungu maana Serikali ikitaka kuvunja mkataba na Acácia gharama kubwa zitatuusu.
#Lakini pia kuendeleza uvyama utatugharimu sana baada ya Mh.Rais Magufuli angewashilikisha wakina mawakili wasomi waliokuwa wakali Tundu Lissu, Kibatala na Fatuma Karume kwenye mambo muhimu kama haya yeye kaleta Uchama sasa itatugharimu.
Baada ya kusomewa makosa hayo, mshtakiwa alikana na Wakili wa Serikali, Challo amesema upelelezi haujakamilika.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo amerudishwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Tsh. Milioni 5 na imeahirishwa hadi October 16 2017.
TANESCO Kagera ilivyowashukia wezi wa umeme