Yara Tanzania imefungua kituo chake cha saba cha mafunzo mkoani Iringa, kikilenga kuinua tija ya wakulima na kusaidia kilimo endelevu.
Kituo hicho, kilichopo wilayani Kilolo, kina lengo la kutoa elimu ya kilimo na msaada wa ugani kwa wakulima wadogo wadogo kitakachowasaidia wakulima wa mazao mbalimbali kuongeza mavuno na kujenga maisha yenye mafanikio.
Mkurugenzi Mkuu wa Yara Tanzania, Winstone Odhiambo , amesisitiza umuhimu wa ushirikiano na wadau kama Farm For the Future (FFF) na Seed Co. Limited katika kufanikisha hilo akisema kinatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko kwa wakulima, kwa kuwapatia elimu na ujuzi wa vitendo, zana, na usaidizi unaohitajika kufikia kilimo endelevu.
Akizundua kituo hicho Mkuu wa wilaya ya Kilolo Peres Magiri aliyemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Iringa Halima Dendego amesema serikali inatambua mchango wa Yara Tanzania kwani una lengo la kuleta mapinduzi makubwa ya kilimo na hasa mkulima mdogo kwa kuhakikisha anafanya kilimo chenye tija na faida huku akipongeza ushirikiano huo wa wadau wenye nia yakumuinua mkulima.
Aidha Magiri amesema serikali inaendelea kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi,upatikanaji wa masoko,miundombinu ya barabara na ukosefu wa mitaji ili kubadilisha wakulima kutoka kwenye kilimo cha mazoea kufikia kilimo chenye tija kitakachowaongezea uzalishaji,kipato na kuboresha maisha ya Mkulima.
Balozi wa Norway nchini Tanzania, Tone Tinnes amesema nchi yake ina mashikiano makubwa na Tanzania huku akihimiza kuongeza jitihada zaidi katika kilimo kwani bado hakujawa na mafanikio ya kutosha kwenye kilimo hasa katika uzalishaji huku Tanzania ikiwa na fursa kubwa yakufanya makubwa zaidi kwenye kilimo kwa kusisitiza matumizi sahihi ya mbolea na virutubishi kutoka Yara Tanzania na Mbegu zenye ubora kutoka Seed Co.Limited.