Dirisha la usajili katika ligi ya Tanzania linatarajiwa kufunguliwa hivi karibu, na baadhi ya vilabu vimeanza harakati za kuimarisha vikosi vyao.
Wakati kukiwa na taarifa kwamba klabu ya Yanga imemtema mshambuliaji Jaja kutoka Brazil, leo hii klabu hiyo imesema kwamba kiungo mkabaji Mbrazil, Emerson De Oliveira Neves Rouqe anatarajiwa kuwasili siku ya Jumanne mchana Dar es salaam kwa ajili ya majaribio na Klabu Yanga na endapo atafuzu moja kwa moja atajiunga na mabingwa hao mara 24 wa Ligi Kuu Tanzania bara.
Emerson mwenye umri wa miaka 24 ambaye kwa sasa anachezea timu ya Bonsucesso FC iliyopo ligi daraja la pili Brazil, msimu uliopita alikuwa akicheza soka la kulipwa nchini Poland katika timu ya Piotrkow Trybunalski FC iliyopo Ligi Daraja la pili.
Ujio wa Emerson kuja kufanya majaribio nchini unakuja kufuatia mshambuliaji wa kimataifa kutoka nchini Brazil pia Geilson Santos “Jaja” kushindwa kurejea nchini baada ya kwenda kwao Brazil na kutoa taarifa kwamba hataweza kurejea tena nchini kutokana kukabiliwa na matatizo ya kifamilia.
Awali ilikuwa familia ya Jaja ije nchini katika kipindi cha mapumziko, lakini waliomba yeye aende Brazil na baada ya kufika huko matatizo ya kifamilia aliyokutana nayo yamepelekea kushindwa kurudi kuitumikia klabu yake na kuomba abakie kwao kwa ajili ya kutatua matatizo hayo.
Kuondoka kwa Jaja kunafanya klabu ya Yanga kubakia na wachezaji wanne tu wa kimataifa ambao ni Mbuyu Twite, Haruna Niyonzima, Hamis Kizza na Andrey Coutinho hivyo endapo Emerson atafuzu atakua anakamilisha idadi ya wachezaji watano wa kimataifa
Endapo Emerson atafuzu majaribo pamoja na vipimo atajiunga na kikosi cha kocha Mbrazil Marcio Maximo katika nafasi ya kiungo mkabaji ikiwa ni sehemu ya kuboresha timu kuelekea kwenye michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom pamoja na mashindano ya kimataifa.
Aidha kikosi cha Yanga baada ya kuwa mapumzikoni kwa takribani wiki mbili, kinatarajiwa kuanza mazoezi siku ya jumatatu katika Uwanja wa shule ya sekondari Loyola kujiandaa na mchezo wa ‘Nani Mtani Jembe’ pamoja na mzunguko wa nane wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara.