BEKI wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani ‘Vidic’, ameibuka na kudai kuiua Al Ahly kwao inawezekana kabisa, lakini itakuwa hivyo kama tu wachezaji wote watacheza kwa ushirikiano na kusaidiana uwanjani pindi mambo yanapokuwa magumu.
Mchezaji huyo mahiri ambaye aliondoka jana Jumatano usiku na kikosi cha timu hiyo kwenda Misri, anaamini kwa kasi waliyonayo katika safu ya ushambuliaji, lazima washinde mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaofanyika Jumapili wiki hii nchini Misri.
Yondani alisema kila kitu kinawezekana kama wachezaji wote wataingia uwanjani na kucheza kwa kujitolea.
“Tumefanya mazoezi vizuri na tupo tayari kwa mapambano, sisi ni kama wanajeshi, tunakwenda vitani hatuhofii chochote, tutahakikisha tunapambana vilivyo kuhakikisha tunashinda mechi hiyo na kukomesha utawala wa wapinzani wetu,” alisisitiza.
“Sioni kitu cha kuhofia kwani hapa nyumbani wengi hawakutupa nafasi ya kushinda, lakini tukashinda (bao 1-0) hivyo hata ugenini tunaweza kushinda hasa kama kila mchezaji atatambua majukumu yake uwanjani.
“Tunapaswa tukacheza kwa umoja na ushirikiano na yeyote atakapoona mwenzake mambo yamemzidi, basi mara moja achukue jukumu la kumsaidia ili kuhakikisha malengo yetu yanatimia.”
Katika mchezo wa kwanza uliofanyika jijini Dar es Salaam, Yanga ilishinda kwa bao lililofungwa na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ katika dakika ya 82. Kwenye marudiano hayo, timu hiyo ya Jangwani inahitaji ushindi au sare ya aina yoyote ili iweze kuwatoa mabingwa watetezi hao na kusonga mbele.
SOURCE: MWANASPOTI