Mamlaka ya Mawasiliano nchini Uganda imeandikia Google, jukwaa la kushirikisha video, kuomba ifunge vituo 14 vinavyodaiwa kuhusishwa na ghasia za mwezi uliopita ambazo zilisababisha vifo vya zaidi ya watu 50.
Ghasia zilizuka katika mji mkuu wa Uganda, Kampala na miji mingine mikuu kufuatia kukamatwa kwa mgombea wa urais wa upinzani na mwanamuziki, Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine, kwa kukiuka masharti ya kudhibiti ugonjwa corona.
Baadhi ya vituo vya habari vyenye chaneli ya YouTube vinavyohusishwa na Bobi Wine ndivyo vinalengwa, lakini mkuu wa masuala ya sheria wa Tume ya Mawasiliano ya Uganda ameambia kituo cha televisheni cha Bloomberg kwamba ni “bahati mbaya” tu.
Katika barua yake kwa Google, Tume hiyo ilisema vituo hivyo vilitumiwa kuchochea virugu na vinatangaza maudhui yanayokiuka sheria, Gazeti la Daily Monitor limeripoti.
Raia wa Uganda wanajianda kushiriki uchaguzi mkuu wa urais na ubunge Januari 14. Rais Yoweri Museveni, ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya miongo mitatu, inataka kuchaguliwa tena.