Leo December 30, tunayo story kutokea kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ambapo imetangaza kumchukulia hatua za kinidhamu Afisa Misitu wa wilaya ya Korogwe aliyeonekana kwenye ‘Clip’ inayosambaa mitandaoni akibishana na abiria aliyekuwa akisafirisha vitanda viwili vya mbao.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano kwa Umma cha (TFS) imemuomba radhi abiria huyo na Watanzania kwa tukio hilo na usumbufu uliojitokeza, huku ikieleza kuwa haina nia ya kuzuia utengenezaji,usafirishaji na matumizi ya samani za mbao mahali popote nchini.
Katika taarifa hiyo imebainisha kuwa, Afisa huyo alimtaka abiria huyo kuonesha Hati ya Kusafirishia (Transit Pass) ya bidhaa hizo kwa mujibu wa Kanuni ya 13(4) ambayo inakataza mwenye chombo chochote cha usafiri kusafirisha mazao ya misitu ambayo hayana hati ya usafirishaji ambapo abiria huyo hakuwa nayo.
“Hata hivyo, Afisa wetu alishindwa kutafsiri masharti ya kifungu hiki na mahitaji ya utoaji wa Hati ya Usafirishaji kwani kama msafirishaji binafsi kwa matumizi ya nyumbani asingeweza kukidhi vigezo vya kuwa na hati hiyo,”imesema taarifa hiyo.
Kutokana na hatua hiyo, TFS imebainisha kuwa hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa mujibu wa Kanuni za utumishi wa umma dhidi ya mtumishi aliyehusika na utoaji wa lugha isiyo na staha wakati akitekeleza sheria ya misitu ambapo alitegemewa kutoa elimu stahiki kwa umma.