Mgogoro wa mwaka mzima sasa baina ya majenerali wa kijeshi wanaoongoza Jeshi la Sudan (SAF) na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) umepelekea kuvurugika mfumo wa elimu na kufutika nafasi za masomo za zaidi ya asilimia 90 ya watoto milioni 19 wenye umri wa kwenda skuli nchini humo.
Taarifa hiyo imetolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) ambalo limeongeza kuwa, Sudan kwa sasa ina mgogoro mbaya zaidi ya elimu duniani, mgogoro ambao utasababisha matatizo makubwa kwa vizazi vijavyo vya Sudan. Mgogoro wa vita unaoendelea nchini Sudan umesababisha uharibifu mkubwa katika mfumo wa elimu wa Sudan.
Takwimu rasmi za Wizara ya Elimu ya Juu ya Sudan zimesema kuwa, vita hivyo vimepelekea zaidi ya vyuo vikuu 100 vya umma na binafsi kufungwa na vimeharibu idadi kubwa ya vyuo vikuu na taasisi za juu.
Katika taarifa yake ya hivi karibuni kwa vyombo vya habari, Waziri wa Elimu wa Sudan, Mahmoud Siral-Khatim Al-Houri alisema kuwa, asilimia 40 ya taasisi za elimu katika Jimbo la Khartoum ambako ndiko vita vilikoanzia, zimeharibiwa.
Msemaji wa Chuo Kikuu cha Zalingei cha makao makuu ya Jimbo la Darfur ya Kati, Al-Hafiz Khamis Ismail, amesema kuwa, kwa uchache asilimia 10 ya walimu wa chuo kikuu hicho wamekimbilia nje ya Sudan.