Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza mradi wa Shilingi Bilioni 11.18 wa kusambaza umeme katika vitongoji 90 utakaonufaisha Kaya 2,970 Mkoani Shinyanga.
Msimamizi wa Miradi ya REA Kanda ya Magharibi, Mhandisi Robert Dulle amebainisha hayo Novemba 05, 2024 Mkoani Shinyanga mbele ya Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anamringi Macha wakati wa kumtambulisha Mkandarasi aliyeshinda zabuni ya kutekeleza mradi huo Kampuni ya wazawa ya Derm Group (T) Limited ya Jijini Dar es Salaam.
“Tunamshukuru Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kiasi cha shilingi 11,184,759,397.2 kitumike kusambaza umeme katika vitongoji 90 Mkoani hapa, leo hii tumefika hapa kumtambulisha Mkandarasi na tayari maandalizi ya awali ya kutekeleza mradi yameanza,” alisema Mhandisi Dulle.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha aliipongeza REA kwa kutekeleza majukumu yake kwa uwazi na kwa utaratibu iliyojiwekea wa kutambulisha wakandarasi kwa viongozi wa Mkoa na Wilaya kote nchini.
“Ujio wenu hapa ni habari njema sana kwa mustakabali mzima wa maendeleo ya Mkoa wetu; pamoja na huduma zingine za jamii huduma ya umeme imepewa kipaumbele kikubwa na Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, umeme ni injini ya uchumi hili halina ubishi na sasa matumizi ya umeme yameongezeka, mahitaji kwa ajii ya majumbani na pia kiuchumi,” alisema Mhe. Macha
Alisema Mkoa wa Shinyanga unaendelea kukua kwa kasi na kwamba kwa sasa shughuli za kiuchumi zimeongezeka ikiwemo uwepo wa viwanda vidogo na vikubwa ambavyo vyote vinahitaji umeme.
“Hapa Shinyanga mbali na madini pia tunashughulika na kilimo cha mpunga na tungependa kuona mkulima akiongeza thamani ya mazao yake hukohuko unapozalishwa mpunga kwa kukoboa na kupata mchele na hapa faida itaongezeka sambamba na kuandaa ajira na fursa zingine vijijini,” alisema.
Aidha, alimtaka Mkandarasi kuhakikisha anatekeleza mradi kwa ubora na anakamilisha kwa wakati kwani tayari miundombinu ipo hivyo hakuna changamoto yoyote itakayokwamisha utekelezaji wa mradi.