Umoja wa mataifa unasema zaidi ya watu 123,000 wamepoteza makazi yao katika ukanda wa Gaza tangu kuzuka kwa mapigano kati ya wapiganaji wa Palestina na wanajeshi wa Israeli.
Wengine zaidi ya 73,000 wamepewa hifadhi katika maeneo ya shule na wengine wakiwa katika makazi ya muda ya dharura.
Israel imekuwa ikitekeleza mashambulio katika ukanda wa Gaza tangu Jumamosi baada ya wapiganaji wa Hamas kurusha makombora kuelekea Israel.
Raia zaidi ya milioni mbili wa Palestina wanaishi katika eneo la Gaza, ambalo limezingirwa na Israel tangu Hamas kuchukua mamlaka mwaka 2007.
Haya yanajiri wakati huu mataifa mbalimbali yakiendelea kutoa wito wa kusitishwa kwa makabiliano hayo, China ikilaani machafuko yanayotekelezwa dhidi ya raia katika ardhi ya Israel na Palestina.
Iran nayo imetupilia mbali madai kuwa inahusika katika tukio hilo la kundi la Hamas kuishambulia Israel.