Zaidi ya shilingi bilioni 200 zinahitajika ili kuzalisha vitabu vya kiada kwa lengo la kufanikisha uwiano wa kitabu kimoja kwa kila mwanafunzi, kuanzia elimu ya maandalizi hadi sekondari.
Kutokana na hitaji hilo, wadau wa elimu nchini wameombwa kuchangia kiasi hicho cha fedha ili kuisaidia Serikali kufanikisha mpango huo muhimu kwa maendeleo ya sekta ya elimu.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali (WEMA), Dk. Mwanakhamis Adam Ameir, amesema wizara hiyo ipo tayari kushirikiana na Taasisi ya Elimu ya Tanzania (TET) kwa kutoa mchango utakaosaidia kuchapisha vitabu hivyo.
Akizungumza katika kikao baina ya TET na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara hiyo, Mazizini Zanzibar, Dk. Ameir alieleza kuwa WEMA inathamini juhudi za taasisi hiyo na itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha kila mwanafunzi anapata vitabu vya kujifunzia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Elimu ya Zanzibar, Abdalla Mussa, alisema kuwa TET ni mdau muhimu wa elimu nchini anayechangia upatikanaji wa vitabu na vifaa vya kujifunzia kwa wanafunzi wa Zanzibar.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Tanzania, Dk. Anneth Komba, alisema kuwa katika kuadhimisha miaka 50 ya taasisi hiyo, watahakikisha wanakusanya fedha ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika uchapishaji na usambazaji wa vitabu vya kiada kuanzia elimu ya maandalizi, msingi hadi sekondari.