Takriban tembo 160 wamekufa huku hali ya ukame ikiikumba Zimbabwe, na huku hali ya hewa ya joto na ukame ikiendelea, wahifadhi wanahofia kunaweza kuwa na vifo zaidi vijavyo.
Tembo hao walikufa kati ya Agosti na Desemba mwaka jana katika hifadhi ya taifa ya Hwange yenye ukubwa wa kilomita za mraba 14,651, ambayo ni makazi ya tembo, nyati, simba, duma, twiga na wanyama wengine walio katika hatari ya kutoweka. Takriban ndovu wengine sita wamegunduliwa hivi karibuni wamekufa nje ya hifadhi katika matukio yanayoshukiwa kuwa ya ujangili.
Mamlaka ya Usimamizi wa Mbuga na Wanyamapori ya Zimbabwe (Zimparks) ilithibitisha vifo vya tembo hao katika mbuga hiyo, na kuvihusisha na ukame.
Tinashe Farawo, msemaji wa Zimparks, alisema Jumanne: “Tumekuwa tukifanya vipimo, na matokeo ya awali yanaonyesha kuwa walikuwa wakifa kutokana na njaa. Wanyama wengi walikuwa wakifa kati ya mita 50 na 100 kutoka vyanzo vya maji.
Tembo waliokufa wengi wao walikuwa vijana, wazee au wagonjwa, mbuga hiyo ilisema.