Zaidi ya wakimbizi 1,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wamekimbilia Uganda kufuatia mashambulizi ya hivi karibuni ya waasi wanaoshukiwa kuwa wa Allied Democratic Forces (ADF).
Shirika la Msalaba Mwekundu la Uganda (URCS) kimetangaza habari hiyio na kuongeza kuwa, wakimbizi hao wameingia Uganda kupitia wilaya ya mpakani ya Bundibugyo ya Mkoa wa Magharibi wa Uganda.
Irene Nakasiita, msemaji wa URCS amesema: “Maafisa wa Wilaya ya Bundibugyo wametangaza kuwa, wamewapa hifadhi wakimbizi hao katika Kituo cha Usafiri cha Bubukwanga ili kuruhusu serikali na washirika wengine kutoa msaada wa kibinadamu kwa wakimbizi hao.”
Ameongeza kuwa, wakimbizi hao wapya wamesajiliwa kama ilivyo utaratibu, na kwa upande wake,Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Uganda URC limetoa huduma ya kwanza ya haraka kwa waliojeruhiwa na baadaye kuwapeleka kwenye kituo cha afya cha eneo hilo kwa huduma zaidi.