Zaidi ya watoto milioni 1.6 walio chini ya umri wa miaka mitano wako katika hatari ya utapiamlo nchini Sudan Kusini mwaka 2024, hasa kutokana na athari za mafuriko, Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) lilionya Jumatatu.
Nchi changa zaidi duniani, Sudan Kusini imekuwa ikikumbwa na misukosuko ya kudumu na ghasia za kikabila tangu ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Sudan mwaka 2011.
Nchi hii yenye takriban watu milioni 11 pia inakabiliwa na hali mbaya ya hewa, ikiwa ni pamoja na mafuriko makubwa yenye athari zinazoweza kuangamiza mamilioni ya watu.
“Tunaona ongezeko la kutisha sana la utapiamlo”, kutokana na mafuriko na msongamano wa watu unaosababisha katika baadhi ya maeneo, alisema Mary-Ellen McGroarty, Mkurugenzi wa WFP nchini Sudan Kusini, katika taarifa kwa vyombo vya habari, akiongeza: “Watoto wadogo. wanateseka zaidi.”
“Zaidi ya watoto milioni 1.6 walio chini ya umri wa miaka mitano wanatarajiwa kukumbwa na utapiamlo mwaka 2024”, iliongeza taarifa hiyo.
Mwezi Mei, UNICEF ilikadiria kuwa utapiamlo utatishia watoto milioni 1.4 ifikapo 2023.
Taarifa kwa vyombo vya habari inahusu hasa hali katika kaunti ya Rubkona (kaskazini), ambapo maji yamezamisha ardhi kubwa, na kulazimisha jamii nzima kuishi kwenye visiwa vidogo tangu 2021. Gharama ya vyakula vya msingi imeongezeka kwa zaidi ya 120 % tangu Aprili.
“Huu ndio ukweli wa maisha katika mstari wa mbele wa mgogoro wa hali ya hewa,” anasema Mary-Ellen McGroarty.
Mgogoro huo umezidishwa na wimbi la mamia kwa maelfu ya raia wa Sudan Kusini wanaokimbia vita nchini Sudan, ambao wanajikuta katika hali ya “dharura ya chakula”.