Wizara ya Afya ya Sudan imesema tokea mwezi August zaidi ya watu 100 wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa wa kipindupindu na dengue katika nchi hiyo iliyokumbwa na vita.
Wizara hiyo imeongeza kuwa kati ya jumla ya visa 1,049 vya ugonjwa wa kipindupindu, 73 kati yake vimesababisha vifo mjini Khartoum, katika Jimbo la Al-Jazira Kusini na Jimbo la Gedaref upande wa magharibi mwa nchi hiyo.
Khartoum imekuwa uwanja wa mapigano makali kati ya wafuasi wa majenerali hasimu, ambayo yameikumba nchi hiyo tokea mwezi Aprili.
Mamia ya maelfu ya wakaazi wa Khartoum wamekimbilia maeneo ya utulivu ya Gedaref na Al-Jazira, na kupelekea maeneo hayo kukabiliwa na uhaba wa maji safi ya kunywa.
Wizara ya Afya ya Sudan pia imesema majimbo tisa ya Sudan yamerekodi visa vya maradhi ya dengue yanayoenezwa na mbu, ambapo vifo 49 vimerikodiwa kati ya visa 3,316.