Serikali ya Nigeria imelazimika kupelekea maafisa wa usalama katika jimbo la Benue nchini Nigeria baada ya kuzuka mapigano makali kati ya makundi hasimu ya wanamgambo na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 40.
Vyombo vya habari vya eneo hilo vimeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, apigano hayo, ambayo yalianza juzi Jumanne, yameenea kwa kasi.
Shirika rasmi la Habari la Nigeria (NAN) nalo limethibitisha habari hiyio na kusema kuwa, mapigano hayo yametokea kwenye eneo la Gbagir lililoko chini ya serikali ya mtaa ya Ukum huko Benue.
Wakaazi wa eneo hilo wameripotiwa kukwama katikati ya mapigano hayo ya umwagaji damu, huku vita vikizidi kuwa vikali kati ya makundi ya wanamgambo ambayo hayakutajwa majina.
Vyombo vya habari vimeripoti kuwa wengi wa wahanga wa mapigano hayo ni wanachama wa vikundi vya wanamgambo hasimu.
Duru za ndani ya Nigeria zimesema kuwa mapigano hayo yalianza kwa sura ya shambulio la kulipiza kisasi lililofanywa na kundi moja la wanamgambo ambao waliamua kulipiza cha kuteswa baadhi ya wakaazi wa eneo hilo na jamii jirani.