Zaidi ya watu 50 wamefariki kutokana na mafuriko katika baadhi ya maeneo nchini Uhispania huku mvua kubwa ikinyesha na kugeuza mitaa kuwa mito na kutatiza huduma za usafiri.
Dhoruba za mvua Jumanne zilifunika maeneo ya kusini na mashariki mwa nchi, pamoja na eneo la Costa del Sol huku miji ya Valencia na Malaga yote ikiathiriwa.
Picha zilionyesha wafanyikazi wa dharura wakipita kwenye maji ya rangi ya matope kuokoa watu, huku magari na gari zikionekana kukwama. Zaidi ya wanajeshi 1,000 kutoka vitengo vya kukabiliana na dharura vya Uhispania wametumwa katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi.
Siku ya Jumatano asubuhi, serikali ya eneo la Valencia, ilithibitisha kuwa watu 51 walifariki katika mafuriko hayo.
Carlos Mazon, kiongozi wa eneo la Valencia, aliuambia mkutano na waandishi wa habari baadhi ya watu walibaki kutengwa katika maeneo yasiyofikika huku msako ukiendelea kwa wale ambao hawajulikani waliko.