Ofisi ya Umoja wa Mataifa Inayoratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema, watu milioni 6.9 nchini Somalia watahitaji msaada wa kibinadamu mwaka ujao.
OCHA imesema, idadi hiyo ni pungufu kutoka asilimia 16 ya mwaka jana, na inalenga watu milioni 5.1 mwaka 2024, na inahitaji dola za kimarekani bilioni 1.7.
Katika ripoti yake ya hivi karibuni kuhusu mpango kazi wa kibinadamu kwa mwaka 2024 nchini Somalia, OCHA imesema msaada wa kibinadamu umezuia hali mbaya ya ukosefu wa usalama wa chakula na lishe bora katika maeneo mengi, lakini changamoto kadhaa ziliibuka, ikiwemo uhaba wa fedha katika sekta zote.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wakati Somalia imefanikiwa kuepuka janga la ukame mwishoni mwa mwaka jana na mwanzoni mwa mwaka huu, watu karibu milioni 4 wameendelea kukabiliwa na uhaba wa chakula na wanahitaji msaada.