Waziri wa Elimu Visiwani Zanzibar Bi. Lela Muhamed Mussa, amepiga marufuku matumizi ya rangi za upinde (Rainbow) katika shule kwa kuhusisha rangi hizo harakati za wapenzi wa jinsia moja.
‘’Busara tumeona ni vyema kuondoa rangi ya upinde katika shule zote za serikali na binafsi, tubadilishe zile nembo, kwasababu hao wenzetu ambao wapo katika mrengo huo wamekua wakizitumia, ili kuwanusuru vijana wetu’’ anasema Bi Lela.
Waziri huyo alibanisha marufuku hiyo wakati akitoa taarifa ya uchunguzi kuhusiana na kamati iliyoundwa kuchunguza tuhuma za shule moja kujihusisha na mafunzo ya wapenzi wa jinsia moja.
Amesema Wizara imejiridhisha kutokuwepo na vitendo vinavyoashiria tuhuma hizo ndani ya Shule hiyo baada ya kufanya uchunguzi kuanzia umiliki wa shule, vifaa vinavyotumika, taaluma za walimu pamoja na njia wanazotumia katika kufundishia na kuona hakuna dalili ya tuhuma zilizotolewa.
Miezi michache iliyopita serikali ya Tanzania ilipiga marufuku vitabu 16 vya mfululizo wa vitabu vya watoto kutumika shuleni kwa madai ya kutetea haki za wapenzi wa jinsia moja -LGBTQ.
Mfululizo wa Diary of a Wimpy Kid unasemekana kukiuka mila, desturi na tamaduni za nchi.
Waziri wa Elimu Adolf Mkenda alisema kuwa vitabu hivyo vinahatarisha ubora wa elimu kwa watoto.