Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeruhusu uingizwaji wa zao la ndizi nchini sambamba na kuchukua tahadhari juu ya magonjwa mbali mbali yanayoathiri zao hilo
Alisema mwaka 2007 Serikali ilitangaza marufuku ya kutoingiza mmea wa migomba na mazao yake zikiwemo ndizi kwa Madhumuni ya kuikinga Zanzibar isishambuliwe na maradhi ya mnyauko wa migomba yaliyoonekana katika maeneo ya kanda ya ziwa ikiwemo mikoa ya Kagera, Bukoba na Mara
Shamata alieleza kuwa serikali ilieleza kuwa maradhi hayo yana uwezo wa kuangamiza asilimia 100 ya uzalishaji wa zao hilo hivyo kuomba ushirikiano kwa wadau ili kukwepa kuingiza maradhi hayo ndani ya Zanzibar
“Nataka niwaambie kuwa tahadhari iliyowekwa imepelekea kuwa na uhaba mkubwa wa bidhaa hiyo sokoni kwa kipindi cha takriban miaka 17 jambo ambalo limesababisha Changamoto mbali mbali kwa Wakaguzi wa Mazao, Wafanyabiashara na wadau wengne katika utekelezwaji wa tahadhari hiyo”, alisema Shamata
Hata hivyo alifahamisha kuwa pamoja na tahadhari zinazoendelea, Serikali inaruhusu uingizwaji wa zao la ndizi kwa mujibu wa sheria ya karantini ya mmea na mazao nambari 9 ya mwaka 1997 kwa utaratibu maalum ili kupunguza changamoto iliyojitokeza.
“Wafanyabiashara wanaoruhusiwa kufanya biashara ya ndizi wanatakiwa kusajiliwa na kupatiwa vibali maalum vya uingizwaji wa zao la ndizi kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo na kupeleka bidhaa hizo kwa Wakaguzi wa Kitengo cha Karantini na Ukaguzi wa Mazao kabla hazijaingia kwenye masoko”, alieleza Shamata