Zimbabwe inashika nafasi ya saba kwa uzalishaji wa almasi duniani ikiwa na pato la kila mwaka la zaidi ya karati milioni 4 zenye thamani ya dola milioni 420 za Kimarekani.
Hayo yameripotiwa na Shirika la Utangazaji la Zimbabwe jana Jumatatu wakati lilipokuwa likinukuu takwimu za hivi karibuni kabisa za uzalishaji wa almasi kutoka kwa taasisi ya KPCS.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, takwimu zinaonesha kuwa, katika upande wa pato la madini ya almasi Zimbabwe iko nyuma ya nchi Botswana, Russia, Angola, Canada, Afrika Kusini na Namibia.
Nchi hiyo ya kusini mwa Afrika inalenga kuzalisha karati milioni 7 za almasi mwaka huu, na shabaha yake hasa ni kufikia mapato ya dola bilioni moja za almasi kila mwaka.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, malengo ya serikali ya Zimbabwe katika upande wa sekta ya madini ni kufikia pato la dola bilioni 12 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa 2023.