Wizara ya Afya ya Zimbabwe Jumapili imethibitisha kesi mbili za kwanza za maambukizi ya mpox bila kueleza kwa kina aina kamili ya virusi hivyo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, kesi ya kwanza ilipatikana kwa kijana wa umri wa miaka 11 ambaye alianza kuonyesha dalili mwezi uliopita baada ya kutembelea Afrika Kusini, taarifa imesema. Kesi ya pili ni ya mwanaume wa umri wa miaka 24 aliyepata maradhi baada ya kusafiri Tanzania. Taarifa zimeongeza kusema kwamba wote wawili wanaendelea kupokea matibabu huku ufuatiliaji wa maambukizi zaidi ukiendelea.
Kesi hizo zililipotiwa mjini Harare na kwenye mji wa kusini wa Mberengwa. Shirika la Afya Duniani Agosti lilitangaza mpox kuwa dharura ya kimataifa kwa mara ya pili ndani ya miaka miwili, wakati aina mpya ya kirusi ikisambaa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hadi kwenye mataifa jirani. Kirusi kipya aina ya ‘clade 1b’ kimeongeza wasi wasi kote duniani kwa kuwa kinasemekana kusambaa kwa urahisi kupitia kutangamana kwa watu.