Kama hukupata nafasi ya kufuatilia kilichokuwa kinaendelea Bungeni Dodoma leo, mambo makubwa matatu ambayo Wabunge walihoji ni haya; kwanza kuhusu IPTL na akaunti ya ESCROW, pili kuhusu mapigano ya wakulima na wafugaji Kiteto na tatu ni suala la mwenendo wa Serikali kusuasua.
Mwenyekiti wa Bunge hilo Mussa Azzan Zungu ametoa majibu haya;- “… Kamati ya uongozi wa Bunge ilikuwa na kikao leo alhamisi tarehe 13 Novemba mwaka 2014, kuanzia saa 7 mchana na kufanya maamuzi muhimu kuhusiana na miongozo iliyoombwa bungeni leo asubuhi kama ifuatavyo. Kuunda kamati teule ya Bunge kushughulikia suala la IPTL na akaunti ya ESCROW.
Katika kujadili mwongozo huu ambao uliombwa na Mheshimiwa Peter Serukamba, kamati ya uongozi imekubaliana na taarifa ilitolewa na serikali kuwa mheshimiwa Waziri Mkuu kesho atakabidhi kwa Spika ripoti ya CAG kuhusu suala hilo, baada ya kupokelewa, utaratibu wa kawaida wa kibunge utafuata kuipatia kamati ya hesabu za Serikali, PAC…”
Kuhusiana na mauaji yaliyotokana na mapigano ya jamii za wakulima na wafugaji Kiteto, mwenyekiti huyo amesema; “…. Katika kujadili suala hili ambalo mwongozo wake uliombwa na David Silinde kamati imeazimia kwamba Serikali kupitia Waziri Mkuu itoe maelezo kwa kamati ya uongozi kesho jioni juu ya jambo hili na namna lilivyoshughulikiwa kuanzia kipindi cha nyuma hadi sasa. Na kisha taarifa kamili kuhusu suala hilo itatolewa Bungeni….”
Suala la tatu ni kuhusu mwenendo wa Serikali kusuasua, Mwenyekiti Zungu amesema; “…. Katika kujadili mwongozo huu ambao ulitolewa Bungeni na Mheshimiwa Rajabu Mbarouk Mohammed, kamati ya uongozi iliazimia kwamba suala hili lijadiliwe katika kikao cha kamati ya uongozi pamoja na Waziri Mkuu kitakachofanyika kesho jioni….”
Kumsikiliza Mwenyekiti wa Bunge akitoa taarifa hiyo bonyeza play hapa.