Zoezi la Uboreshaji la Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora limeingia siku ya pili baada ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa kulizindua Julai 20,2024 katika uwanja wa Kawawa Mkoani Kigoma.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhani alipata fursa ya kukagua baadhi ya vituo vya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la mpiga Kura katika Wilaya za Kasulu za Buhigwe mkoani Kigoma na kujionea hali ilivyo vituoni na mwitikio wa watu katika vituo hivyo.
Akizungumzia uboreshaji huo, Kailima alisema hadi kufikia jana tarehe 21 Julai 2024, hapakua na changamoto yeyote iliyojitokeza katika mikoa yote ya Tabora, Kigoma na Katavi na wananchi wameendelea kujitokeza kwa wingi kujiandfikisha lakini pia kuboresha taarifa zao.
Aidha, Kailima alivipongeza vyama kwa kuweka mawakala katika vituo vya uandikishaji na kuwataka mawakala hao kusaidia utambuzi kwa watu wasio raia wa Tanzania ambao watafika kwaajili ya kuandikishwa.
Kailima alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha wananchi kuwa sasa zimesalia siku tano kati ya saba zilizopangwa kuandikisha wananchi katika mikoa hiyo ya Kigoma, Katavi na Tabora hivyo wananchi wazitumie siku zilizobaki kujitokeza na kujiandikisha.
Amesema vyama vya siasa vinawajibu wa kuwahimiza, wanachama, wafuasi wao kujitokeza kujiandikisha na kuboresha taarifa zao ili waweze kupiga kura katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.