Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) umedhamiria kutumia uzoefu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakzi (WCF) katika kuanzisha Skimu ya Malipo ya Fidia kwa wafanyakazi watakaoumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSSF, Bw. Nassor Shaaban, ameyasema hayo pembezoni mwa Kongamano la Wakuu wa Taasisi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ambalo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar linalofanyika katika viawanja vya Nyamanzi mjini Unguja.
“Katika utayarishaji wetu wa kuanzisha Mafao (skimu) haya ya mfanyakazi atakayeumia kazini, tumekuwa tukishirikiana sana na wenzetu wa WCF ili kupata uzoefu kutoka kwao ambao wana uzoefu wa miaka mingi na wanasifika kwa kutoa mafao mazuri,” amefafanua Bw. Shaaban.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma amesema kama inavyosema Dira ya Mfuko huo ya kuwa Mfano Bora wa Kuigwa Barani Afrika katika Utoaji Huduma za Mafao ya Fidia kwa Mfanyakazi anayeumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi, waliona upo umuhimu wa kuwajengea uwezo wenzao wa Zanzibar ili na wao waweze kuwa na chombo kama hicho.
“WCF imekuwa Mfuko wa kuigwa barani Afrika, ukanda wa SADC na Afrika Mashariki, na kama uzoefu huu tunausambaza katika nchi hizo, tumeona ni vema uzoefu huu pia tuweze kuusambaza kwa ndugu zetu wa Zanzibar na ndio maana tumekua na ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha na wao wanafikia azma yao ya kutoa fao hilo,” amefafanua Dkt. Mduma.
Pamoja na mambo mengine, kongamano hilo lilikuwa na lengo la kuwawezesha wakuu wa taasisi za SMT na SMZ kubadilishana uzoefu na kujadiliana namna ya kushirikiana baina ya taasisi wanazoziongoza.