Top Stories

Ilichobaini Tume iliyoundwa kuchunguza Airtel kumilikiwa na serikali

on

Waziri wa Fedha na Mipango Dr. Philip Isdor Mpango leo January 11, 2018 amewasilisha taarifa ya kamati aliyoiunda ili kuchunguza umiliki wa kampuni ya simu Airtel kwa President Dr. John Pombe Magufuli ambaye aliagiza kufanyika kwa uchunguzi huo tarehe December 20, 2017.

Dr. Mpango amesema Serikali imejiridhisha kuwa ubinafsishaji wa Shirika la Simu Tanzania (TTCL) kwenda Celtel, baadaye kuhamishiwa Zain na sasa Airtel ulifanyika kwa ukiukwaji mkubwa wa sheria, kanuni na taratibu.

Kufuatia ukiukwaji huo Dr. Mpango amesema Serikali inayomiliki asilimia 40 ya hisa za kampuni ya Airtel imeamua kufanya mazungumzo na kampuni ya Airtel inayomiliki asilimia 60 ya hisa ili nchi iweze kupata haki yake.

“Lakini niwaambie Watanzania yale ambayo tumeyaona ni machafu sana, ni mambo ya hovyo kabisa, nchi yetu kwa kifupi tuliingizwa mkenge, ni fedha nyingi zimepotea kwa hiyo sisi katika majadiliano haya lengo letu litakuwa ni kuhakikisha Watanzania wanapata haki yao” Dr. Mpango.

Leo pia Rais Magufuli amepokea taarifa ya utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa tarehe 25 November, 2017 wakati wa ufunguzi wa Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi  (Mloganzila) kutoka kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu.

Maagizo yaliyotekelezwa ni kupunguza baadhi ya idara na madaktari katika hospitali ya Taifa Muhimbili na kuhamishia Mloganzila na hospitali za mikoa kuhamishwa kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwenda Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Ummy Mwalimu amewasilisha taarifa hiyo akiwa ameongozana na  viongozi wakuu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Mifupa (MOI), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKHI), Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi (MUHAS).

Nae Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi amepokea vitabu vya kanuni za sheria ya madini namba 7 ya mwaka 2017 kutoka kwa Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi

Prof. Kabudi ameongozana  Manaibu Waziri wa Madini Stanslaus Haroon Nyongo na Doto Mashaka Biteko, Kabudi amesema kanuni hizo zimekamilika siku moja kabla ya tarehe ya mwisho iliyotolewa na Rais Magufuli na kubainisha kuwa sasa sheria inaweza kuanza kutumika.

Kwa upande wao Manaibu Waziri wa Madini wamewataka Watanzania na wadau wote wa sekta ya madini kushirikiana na Serikali kutekeleza sheria hiyo na wamempongeza Rais Magufuli kwa kutoa msukumo wa kukamilishwa kwa kanuni hizo.

“LOWASSA AMEKATA KIU YAKE, TUNAMSHUKURU RAIS JPM’ MRISHO GAMBO

 

 

Soma na hizi

Tupia Comments