Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuachia huru Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando, baada ya kutomtia hatiani.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi ambapo amesema katika shauri hilo Tido alikabiliwa na mashtaka matano ikiwemo kutumia madaraka yake vibaya na kusababisha hasara kwa TBC zaidi ya Milioni 800.
Katika hukumu hiyo, Hakimu Shaidi amesema kuwa upande wa mashtaka ulileta mashahidi ambapo miongoni mwa mambo yaliyozungumzwa ni suala la mikataba.
Amesema katika ushahidi huo wa mkataba ulionyesha kuna sahihi ya Tido na Channel 2 lakini hakuna sahihi ya Mwanasheria Mkuu, Bodi wala mamlaka nyingine.
Amesema kuwa yeye kama Mkurugenzi alikuwa ana wajibu wa kufata taratibu za zabuni, hivyo ili kitu kiwe mkataba lazima kipitie hatua lakini mkataba huo anaodaiwa kusaini Tido na Channel 2 haina sifa ya kuwa mikataba.
Pia ushahidi hauelezi malipo yamefanyika kwa nani kwa maana hiyo malipo yamefanyika kwa mikataba ambayo haina vigezo.
Amesema kuwa mchakato wa kusaini mikataba hiyo ilikiukwa sana, hivyo ushahidi uliotolewa haujathibitisha kwamba Tido ametiwa hatiani, hivyo anamuachia huru.
Miongoni mwa mashtaka yaliyokuwa yakimkabili, anadaiwa kuwa June 16, 2008 akiwa Dubai,Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Tido ambaye alikuwa Mkurugenzi wa TBC, kwa makusudi alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mkataba wa kuendesha na utangazaji wa vipindi vya televisheni kati ya TBC na Channel 2 Group Corporation (BV1) bila ya kupitisha zabuni, kitu ambacho ni kinyume na Sheria ya Manunuzi na kuinufaisha BVl.
BREAKING: JAJI MKUU AMPONGEZA MSAJILI ALIYEIKATAA KESI YA ZITTO KABWE