MWANANCHI
Mawaziri wawili wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete wameanguka kwenye marudio ya Kura za Maoni zilizofanyika juzi, huku matokeo ya Jimbo la Busega yakikwama baada ya Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo, Dk. Titus Kamani kumshambulia msimamizi wa Uchaguzi.
Walioanguka ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid (Rufiji) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mazingira), Dk. Binilith Mahenge (Makete), huku Dk Raphael Chegeni akiongoza kwenye Jimbo la Busega.
Dk Kamani na wafuasi walizuia matokeo kutangazwa na kuibuka kwa vurugu zilizosababisha polisi kuingilia kati na kukamata watu wanne walioonekana kumuunga mkono.
“Aliyeshinda ameshinda tu hakuna namna. Kilichofanywa na Waziri Kamani kumpiga msimamizi huyo ni mambo ya binadamu tu… lakini walioshindwa lazima wakubali matokeo na lazima yatangazwe,” alisema Paul Mzindakaya, Mkuu wa Wilaya ya Busega.
Vurugu zilianza saa 4 asubuhi baada ya Dk Kamani, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Simiyu, kuingilia kati wakati Mabiya, ambaye ni katibu wa Wilaya ya Meatu, akianza kutangaza matokeo.
Baada ya Polisi waliokuwa na silaha kuimarisha ulinzi, Mabiya alisimama kutangaza matokeo lakini akakatishwa baada ya kurukiwa na watu walioonekana kumuunga mkono Waziri Kamani na kupigwa makonde mbele ya Polisi na Mzindakaya.
Kipigo hicho kilimfanya Mabiya akimbilie ndani ya ofisi za chama hicho na kuacha askari wa Kikosi cha FFU wakitumia nguvu kudhibiti watu hao.
Wakati wote wa vurugu hizo, Dk. Chegeni alikuwa amesimama pembeni mwa ofisi za chama hicho akishuhudia matukio hayo, lakini baadaye akaondoka akiwa amepanda gari lake huku akishangiliwa.
Baada ya polisi kufanikiwa kutuliza ghasia, Mabiya alisimama tena kutangaza matokeo hayo, lakini Dk Kamani alimfuata na kumshambulia kwa makonde, kukazuka tafrani kubwa zaidi.
MWANANCHI
Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), limemwonya Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika kutolihusisha na siasa, huku likikana kuwanyang’anya kadi za kupigia kura maofisa wake ili kufanya hujuma katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Nae Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Ernest Mangu amesema suala hilo linapotoshwa na kuwa ni wajibu wa viongozi wa Jeshi hilo kuhakikisha Askari wote wanatumia fursa ya kumchagua kiongozi wao.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Habari na Uhusiano kwa Umma, Kanali Ngemela Lubinga alisema Jeshi limesikitishwa na kauli ya Mnyika ya kwamba limewanyang’anya kadi za kupigia kura maofisa wake .
“Wanajeshi hawaruhusiwi kabisa kuwa wanachama wa chama chochote cha siasa,”– Kanali Lubinga.
Mbunge John Mnyika alisema CHADEMA imebaini uwapo wa mbinu za kutaka kuhujumiwa kwenye Uchaguzi Mkuu kwani Serikali imeviagiza vyombo vya usalama, kupeleka namba za vitambulisho vya askari wote kwa wakuu wa vitengo jambo ambalo ni kinyume na utaratibu.
NIPASHE
Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC imetangaza siku ya urejeshaji fomu za Urais na Makamu wa rais kuwa ni AlhamisI ijayo huku ikipiga marufuku maandamano, ni watu saba tu ndio wataruhusiwa kusindikiza Wagombea.
Urejeshaji fomu utaanza saa 1:30 asubuhi hadi saa 10:00 jioni, huku wagombea wote wakitakiwa kufika kwenye ofisi za Tume wakisindikizwa na watu hao na majina yao yanatakiwa yawasilishwe Tume kabla ya Agosti 20, ili kuratibu kazi hiyo.
“Wagombea hawaruhusiwi kuja Tume kwa maandamano, shamrashamra, nderemo wala vifijo. Hii ni kwa sababu siku hiyo vyama vya siasa vitakavyowasilisha fomu za kuomba uteuzi vitakuwa vingi hivyo kila chama kikija Tume kwa maandamano na shamrashamra kunaweza kutokea uvujifu wa amani,“– Mkurugenzi wa NEC, Ramadhani Kailima.
Alisema sababu nyingine ya kuanga hivyo ni kuwawezesha wananchi wengine kuendelea na shughuli zao pamoja na kuimarisha amani na utulivu.
NIPASHE
Hali inazidi kuwa tete ndani ya Chama cha CCM baada ya vigogo tisa, akiwamo Mwenyekiti wa Jumuiya ya UVCCM Vijana Mkoa wa Kilimanjaro (UVCCM), Fredy Mushi jana kujiuzulu nyadhifa zao na kutangaza kujiunga na CHADEMA.
Wengine waliotimka ni Katibu wa Uchumi na Fedha na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa CCM, Paul Matemu, Mchumi wa UVCCM Mkoa wa Kilimanjaro, Jerome Komu na Noel Nnko ambaye alikuwa Mratibu wa Kanda ya Kaskazini wa Marafiki wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, wamo pia Wafanyabiashara maarufu wa mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, Douglas Malamsha na Peter Kirenga.
Kujitoa kwa vigogo hao, kumefanya idadi ya makada waliokihama CCM ndani ya mwezi mmoja kufikia 21.
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amesema CCM hakishtushwi na makada na viongozi wanaoendelea kukihama chama hicho na kujiunga na CHADEMA na kudai kuwa wanaoondoka wana sababu zao binafsi.
Amesema hakuna kiongozi wa upinzani ambaye hakuanzia CCM hivyo ni hali ya kawaida kwa chama kikubwa kama hicho ambacho kina mtaji wa wanachama takribani milioni nane, makada wake kuhama.
“Waliohama, wanaohama na watakaohama hili siyo jambo jipya lilishatokea tangu miaka 23 iliyopita na litaendelea kwa muda mrefu hivyo siyo jambo la kushangaza, kuna viongozi wakubwa waliondoka na wengine wakarudi, Mfano Maalim Seif na Agustine Mrema walikuwa CCM na waliondoka”—Nape Nnauye.
Nape alikanusha taarifa zinazosambaa mitandaoni kuwa, Mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, alitangaza kuwagawia kompyuta walimu wote.
Alisema taarifa hizo ni za uzushi na kwamba Ilani ya uchaguzi ya chama hicho ilipitishwa juzi mkoani Dodoma na inatarajiwa kuzinduliwa Agosti 23, mwaka huu.
HABARI LEO
Jeshi la Polisi Dodoma linamshikilia mtu mmoja Mohammed Abdallah baada ya kukutwa akitoa huduma za kidaktari ambazo hana utaalamu nazo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema Abdallah alikamatwa Agosti 12 Wilaya ya Kongwa, akiwa tayari ametoa huduma ya matibabu kwa wagonjwa zaidi ya 20.
Kamanda Misime alisema baada ya mtuhumiwa kukamatwa katika nyumba hiyo alikopanga, alipekuliwa na kukutwa na dawa mbalimbali zenye nembo ya Bohari ya Madawa (MSD), mifuko tisa, sindano na baadhi ya vifaa tiba vinavyodhaniwa vilipatikana kwa njia isiyo halali.
Baada ya kuhojiwa mtuhumiwa alikiri kutenda kosa hilo na kuongeza kwamba hana taaluma yoyote ya utabibu na elimu yake ni darasa la saba, Kamanda Misime alisema uchunguzi zaidi unaendelea na ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani.
UHURU
Jeshi la JWTZ limesema Askari wake watappiga Kura kwenye Vituo vya Uraiani na sio ndani ya Kambi za Jeshi.
“Wanachama hawaruhusiwi kuwa Wanachama wa Chama chochote cha Kisiasa, hawaruhusiwi kuwa mashabiki wa Chama chochote”—alisema Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa JWTZ, Meja Ngomelo Lubinga huku akipinga kauli ya Mbunge John Mnyika kwamba Jeshi hilo limechukua Kadi za Kupigia Kura kwa baadhi ya Askari.
PAPO KWA PAPO zipate habari zote zinazonifikia za siasa muziki, michezo, maisha, Breaking news na nyingine kwa kujiunga hapa na mimi >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos