Hatimaye Wajumbe wa Bunge maalum la katiba wameanza vikao vyao February 18 2014 kwa kuelezwa majukumu yao katika kipindi chote watakachoketi kuipitia rasimu ya pili ya katiba mpya ambayo baadae itaunda Katiba mama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Moja ya jukumu lao kubwa ni kutunza mali za mamlaka ya nchi, kupigavita ubadhirifu, kuhimiza matumizi bora ya rasilimali za nchi huku wakitakiwa kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa na kudumishwa.
Kutokana na hilo, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Bunge la Tanzania Kitorina Kippa, amewataka wajumbe wa bunge maalum kutambua kazi wanayoenda kuifanya kuwa haina mshahara na hakutakuwa na malipo baada ya kuhitimisha kazi hiyo.
Mara baada ya ufafanuzi huo, baadhi ya wajumbe akiwemo DK. AVEMARIA SEMAKAFU na JULIUS MTATIRO wamehoji baadhi ya taratibu ikiwemo kuwepo na usawa wa jinsia kwa viongozi watakaoliongoza bunge hilo maalum.
Bunge hili maalum la katiba lilitarajiwa kumchagua Mwenyekiti wa muda atakayeliongoza kwa mpito ili kumpata Mwenyekiti wa kudumu tayari kwa kuunda kanuni zitakazowezesha kujadiliwa kwa rasimu ya pili ya katiba.